
PROF. NAGU ATOA WITO WA USIMAMIZI MATHUBUTI WA TAKWIMU ZA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) na Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa (RHMT) kuhakikisha wanasimamia kikamilifu upatikanaji wa takwimu bora na sahihi, pamoja na kusisitiza matumizi ya takwimu hizo katika kufanya maamuzi ya kisera na kuboresha huduma za afya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kutathmini utoaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), Malaria na huduma unganishi za afya kilichowakutanisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Wafamasia wa Mikoa, Waratibu wa UKIMWI na Waratibu wa Malaria Jijini Dodoma, Prof. Nagu amesema:
“Ni lazima tutumie vizuri fedha tulizonazo kwa kubuni njia ambazo zitasaidia kupunguza gharama ili kufikia malengo tunayoyahitaji, hivyo Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na RHMT simamieni upatikanaji wa takwimu bora na kusisitiza matumizi ya takwimu hizo” Amesema Prof. Nagu.
Aidha, Prof. Nagu amezitaka Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya ngazi ya Halmashauri (CHMT) kuhakikisha uendelevu wa huduma za msingi, upatikanaji wa vipimo vya maabara, na uhakika wa dawa kwa magonjwa yaliyotajwa na mengineyo, kwa kuzingatia takwimu wanazoziwasilisha.
Pia, Prof. Nagu amewataka Wafamasia kote nchini kuzingatia maoteo sahihi ya dawa katika maeneo yao kulingana na mahitaji ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa na pia kupunguza kuchina (expiry) kwa Dawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amesema kuwa kikao hicho ni muhimu kwani kitatoa fursa ya kujadili masuala muhimu ikiwemo maadili ya utumishi wa umma na nidhamu ya kitaaluma, ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Comments
Please sign in to leave a comment.

