
SUMA JKT WAPEWA SIKU 7 KUKAMILISHA RASIMU YA NYONGEZA YA MKATABA
Na OWM-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, ameipa kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT muda wa siku saba kuwasilisha rasimu ya nyongeza ya mkataba (addendum) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) linalojengwa katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mhe. Kwagilwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, akiwa ameambatana na viongozi wa Tume ya Utumishi wa Walimu akiwemo Mwenyekiti wa Tume na makamishna wake. Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaimarisha utoaji wa huduma kwa walimu nchini.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mhe. Kwagilwa alisema tayari taarifa za awali kuhusu nyongeza ya mkataba zilishawasilishwa na kufanyiwa marekebisho kwa upande wa Serikali, na hivyo mkandarasi anatakiwa kurejesha rasimu iliyoboreshwa ndani ya siku saba.
“Kumekuwepo na mawasiliano kuhusu ‘addendum’. Baada ya kuleta rasimu, tulitoa marekebisho na ikarudi kwenu. Sasa ndani ya siku saba tunataka tuipate rasimu hiyo tayari kwa hatua zaidi,” alisema Mhe. Kwagilwa.
Aidha, amesisitiza kuwa SUMA JKT lazima ihakikishe ujenzi wa jengo hilo unakamilika ndani ya muda wa mkataba utakaoboreshwa, ambao ni hadi Juni 1, 2026.
“Tumekubaliana kuongeza muda wa mkataba na mmetaja kuwa ujenzi utakamilika Juni mwakani. Ni muhimu kuhakikisha hilo linatekelezwa ili kuepusha haja ya kuongeza muda mwingine wa kazi,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania, Paulina Mkwama, amesema Tume itahakikisha inasimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ili ujenzi huo ukamilike kama ilivyopangwa.
Comments
Please sign in to leave a comment.

