
PROF. NAGU AHIMIZA UONGOZI WENYE MATOKEO CHANYA KWA WAGANGA WAFAWIDHI WA HALMASHAURI.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amewataka Waganga Wafawidhi wa hospitali za Halmashauri kuwa viongozi wenye matokeo chanya katika utendeji wao na kusimamia kikamilifu utendaji kazi wa watumishi wao, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Prof. Nagu ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya uongozi na usimamizi kwa Waganga Wafawidhi wa hospitali za Halmashauri na vituo vya afya, yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Mzumbe kupitia Kituo cha Umahiri cha Ufuatiliaji na Tathmini ya Afya (Centre for Excellence in Monitoring and Evaluation), Mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo, Prof. Nagu aliwataka washiriki kuhakikisha wanatumia mafunzo waliyopata kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
“Baada ya mafunzo haya tuone matokeo. Tumia mifumo iliyopo kutatua changamoto, endeleeni kujitathmini mara kwa mara, na tutaona matokeo chanya katika maeneo yenu,” alisema Prof. Nagu.
Aidha, aliwasisitiza washiriki kuandaa mpango kazi baada ya mafunzo, pamoja na kufanya tathmini za mara kwa mara kulingana na vigezo vya upimaji sekta ya afya, ili kuimarisha huduma katika vituo wanavyovisimamia.
Katika hatua nyingine, Prof. Nagu aliwakumbusha Waganga Wafawidhi kuhakikisha watumishi wanapatiwa stahiki zao kwa wakati, ikiwemo posho za kujikimu kwa watumishi wapya, sare, na fedha za uhamisho. Alieleza kuwa hatua hiyo itaongeza morali ya kazi, uwajibikaji, na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma.
Mafunzo hayo yalikusudiwa kujenga uwezo wa viongozi wa afya katika ngazi za Halmashauri, ili kuongeza ubora na ufanisi katika usimamizi wa huduma za afya nchini.
Comments
Please sign in to leave a comment.

