MHE. JAFO AHIMIZA MIKOA KUSIMAMIA LISHE ILI KUPUNGUZA UDUMAVU

Mhe Jafo ahimiza Mikoa kusimamia Lishe
--------------------------------------------------

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) amewaongoza wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara, kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma.

Akiongea na Wakuu wa Mikoa katika ofisi za Wizara hiyo mjini Dodoma, Mhe. Jafo amesema maelekezo hayo awali, yalitolewa na Mhe. Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu, kuhusu tatizo la Lishe katika Mikoa nchini ambalo nchi imekwishajitoa kulishughulikia na kutenga fedha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018.

“Tumesaini hii mikataba kwa lengo kubwa la kuhakikisha kwamba Wakuu wa Mikoa kama ndio viongozi wa Wakuu wa Mikoa, wahakikishe halmashauri zao zinaenda kutekeleza mipango yao ya bajeti ambayo imetengwa katika halmashauri zao kwa lengo kubwa kwamba, tunaenda kutekeleza tatizo la lishe ndani ya halmashauri zetu”

Mhe. Jafo amesema Wakuu wa Mikoa wanayo dhamana kubwa ya kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya na suala la lishe kwa ujumla, hivyo Watendaji watoe taarifa zao kwa Wakuu wa Wilaya kabla ya kuwasilishwa kwa Wakuu wa Mikoa kwa hatua stahiki.

“Wakurugenzi watoe taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Wilaya nao wawasilishe kwa Wakuu wa Mikoa ili waone namna ya kuzisemea taarifa hizo”, katika suala zima la utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza na kuwasimamia Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya masuala ya lishe na ujenzi wa vituo vya afya kwani mpaka sasa jumla ya vituo 2011 vimepanuliwa na kujengwa ili kutoa huduma bora kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe S. Kebwe amesema, anaipongeza Serikali kwa kutoa takribani shilingi 11.6 Bilioni kwa ajili ya suala la lishe hasa katika kipengele cha udumavu.

Aidha, amesema suala zima la upatikanaji wa chakula mkoani Morogoro sio tatizo bali ni elimu ya ulaji chakula ndiyo inapaswa kutolewa ili kupunguza utapiamlo lakini pia kumekuwepo na tatizo la Maafisa Lishe katika halmashauri nchini kupangiwa kazi nyingine, kwa mfano kufanya kazi ya Idara tofauti kama vile kukusanya kodi.

Naye Stephen Motambi, Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI, amesema suala la Lishe limekuwa likifanyika katika Mikoa na Halmashauri zote katika kukabiliana na tatizo hili lakini kwa hivi sasa hali ya udumavu ni asilimia 34 hivyo mikoa inapaswa kuweka mikakati kuhusiana na kuondoa kabisa tatizo la lishe.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.