WAZIRI SELEMANI JAFO ATAKA VIWANDA VIPYA 2600 KATIKA MIKOA 26 IFIKAPO DESEMBA 2018

Na Ismail Ngayonga

WAZIRI SELEMANI JAFO ATAKA VIWANDA VIPYA 2600 KATIKA MIKOA 26 IFIKAPO DESEMBA 2018
--------------------------------------------------

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Seleman Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha kuwa kila mmoja anajenga viwanda vipya 100 kuanzia Desemba 2017 hadi Desemba 2018.

Akizungumza na Wakuu wa mikoa wapya walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, na kufanya nao mazungumzo katika Ofisi ya TAMISEMI Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2018, mikoa yote 26 ya Tanzania Bara inakuwa na viwanda vipya 2600.

Waziri Jafo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kufikia nchi ya uchumi wa kipato cha kati kupitia ujenzi wa viwanda, hivyo aliwataka wakuu wa Mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa wanaibua viwanda vidogo na vya kati kwa kuhamasisha ushiriki wa Viongozi ndani ya mikoa na wananchi wote katika maeneo yao ya utawala.

Aliongeza kuwa katika kusimamia utekelezaji wa agizo hilo, Ofisi yake itaweka utaratibu maalum wa kupima utendaji kazi wa Kila Kiongozi wa Mkoa katika kuangalia ushiriki wake wa kuwajengea hamasa Viongozi wa chini wakiwemo Wakuu wa W ilaya na wananchi.

“Serikali itatoa vyeti kwa Mikoa yote itakayofanya vizuri katika ujenzi wa viwanda, hatua hii inalenga kutoa motisha kwa mikoa iliyobaki kuweza kujifunza na kubaini mbinu mbadala katika kuibua viwanda ili kuweza kuwakomboa kiuchumi wananchi” alisema Jafo.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo alisema katika kufanikisha dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini Serikali inaendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika upatikanaji wa malighafi za kilimo, na hivyo kuwataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Maafisa Ugani wanatekeleza vyema majukumu yao ya kazi.

Aidha Jafo aliwataka Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia vyema makusanyo ya fedha za ndani zinazokusanywa katika Halmashauri zote nchini na kutumia vyema fedha za asilimia 5 zilizotengwa katika halmashauri kuwawezesha na kuhamasisha wananchi kupata mikopo ili kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Waziri Jafo pia aliwataka Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuweza kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika ili weweze kupatiwa mikopo kupitia mifuko ya fedha inayotolewa na Serikali na hivyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima alisema ili kufanikisha dhana ya uchumi wa viwanda, Serikali haina budi kuwapa msukumo na ushirikiano wa karibu Wanasayansi ili kuwawezesha kuibua viwanda vingi zaidi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kilimo nchini.

MWISHO

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.