SERIKALI YAZINDUA PROGRAMU YA TEHAMA KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

Na. Fred J.Kibano

Serikali yazindua matumizi ya tehama mashuleni

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda amezindua Mradi wa Afican Digital Schools Initiative (ADSI) katika shule ya sekondari ya wasichana Kilakala mjini Morogoro na kuwataka Wadau wote kuupoke mradi na kushiriki katika hatua zote za utekelezaji wake.

Akizizindua Mradi huo Bw. Tixon Nzunda amesema Mradi huo, “unalenga kuboresha miundombinu na kuzijengea uwezo shule 40 kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi, Teknolojia, kiingereza na hisabati na hatimaye kuinua ubora wa elimu katika shule na Taifa kwa ujumla”

Amesema Dira ya Taifa ya mwaka 2025 ni kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati na hivyo Ofisi ya Rais TAMISEMI itahakikisha mazingira na vifaa vya kufundishia na kujifunzia yanaboreshwa hali itakayopelekea kutupatia wataalam wa wenye maarifa na ujuzi kwa ustawi wa Tanzania na kwa malengo ya millenia yaliyokusudiwa.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa, shule zote za sekondari na msingi zinafikiwa na mfumo wa utoaji wa elimu kwa njia ya digitali (TEHAMA), Tunaomba Washirika wetu wa Maendeleo, Jamii na Taasisi binafsi kushirikiana na Serikali kufikia lengo hili”

Aidha, Bw. Nzunda amewataka wazazi, wanafunzi, na wanafunzi kutumia vema miundombinu ya TEHAMA iliyowekwa kwa matumizi sahihi katika kutoa elimu kwa watoto ambao ni Taifa la kesho.

“Wito wangu kwenu ni kuhakikisha mnatumia miundombinu na mfumo huu kwa ajili ya kurahisishia utendaji wenu wa kazi, na utumike kwa ajili ya maslahi mapana ya shule zenu”

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu ameiagiza Mikoa na Halmashauri kuhakikisha malengo yaliyowekwa na shirika la Afican Digital Schools Initiative (ADSI) yanafikiwa katika shule za mfano na shule 40 zitakazohusika lengo likiwa ni kuleta matokeo chanya, “Uongozi katika ngazi ya Mkoa na Wilaya hakikisheni kwamba malengo ya mradi wa ADSI yanafikiwa”

Akitoa maelezo ya awali kumkaribisha mgeni rasmi, Meneja Mradi (ADSI) Tanzania Bi. Joyce Msola amesema Mradi wa kutumia TEHAMA yenye tija katika mashule utatekelezwa katika shule za mfano lakini pia itafanyika tathmini ili kuthibitisha kama mradi unaleta matokeo yenye manufaa.

Naye Meneja wa Programu Bw.Senthil Kumar amesema kuwa Mradi wa ‘African Digital Schools Initiative’ unatekelezwa katika nchi tatu barani Afrika Tanzania ikiwa ni mojawapo lengo kuu ni kuweza kujenga miundombinu ya TEHAMA katika shule za mfano ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo kwa walimu, wanafunzi, watumiaji wa TEHAMA na wadau wengine. Kwa hivi sasa unatarajiwa kuanza katika shule mbili za mfano ambazo ni Kibaha sekondari iliyopo mkoani Pwani na Kilakala iliyopo mkoani Morogoro ambapo matarajio ni kuupeleka katika shule nyingine arobaini katika mikoa hiyo.

Kwa upande wake Bi.Renalda Tesha Mkuu mradi huu utakuwa na manufaa kwa Kilakala sekondari kwa kuwa utasaidia takribani wanafunzi wapatao 570 kwa kujifunza masuala yote yanayohusiana na Teknolojia hiyo muhimu na pia kwa walimu utawasaidia kujifunza na kufundishia wanafunzi ili kuendana na karne ya sasa ya sanyansi na teknolojia.

Mradi wa ‘African Digital Schools Initiative’ ni Mradi mpya ambao unatekelezwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na WIzara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Shirika la Global e Schools and Communities (GESCI). Mradi huu utakuwa katika mikoa miwili ya Pwani na Morogoro ukilenga zaidi kuboresha miundombinu ya utumiaji TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.