MHE.JAFO ATOA AGIZO KWA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA, AIPONGEZA HALMASHAURI YA GAIRO

Na.Fred J.Kibano

Mhe Jafo atoa Agizo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini ambayo Halmashauri zao zilipatiwa fedha lakini bado hawajaanza ujenzi mpaka sasa wawasilishe majina ya halmashauri hizo kabla ya Oktoba 10, mwaka huu ili mchakato wa kuzihamisha fedha hizo ufanyike mara moja kwa kuzipeleka fedha hizo katika halmashauri zinazo endelea na ujenzi kwa sasa.

Mhe. Jafo ametoa agizo hilo wakati akifanya ziara yake ya kikazi wilayani Gairo na kusema, “Leo hii natoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakapofika tarehe 10/10/2017 nipate taarifa katika Halmashauri zao, katika mikoa yao, na kama kuna halmashauri haijaanza ujenzi nipate taarifa hiyo, lakini Ofisi ya Rais TAMISEMI tutaenda kuhakiki kila halmashauri mpaka hiyo tarehe 10 Oktoba, na ikifika hapo ndio mwisho, kwamba fedha zote ambazo halmashauri watakuwa hawajatumia tutazihamisha tutapeleka katika halmashauri wanazofanya kazi”, alisisitiza Mhe. Jafo.

Pia amesema takwimu watakazotoa Makatibu Tawala wa Mikoa hao ziwe na uhalisia na kwamba suala hili halitakuwa na mjadala bali ni utekelezaji.

Katika hatua nyingine, Mhe. Selemani Jafo ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoani Morogoro kwa kutekeleza maagizo ya Serikali kwa kufanya maendeleo mazuri ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Halmashauri hiyo ambalo ndilo jengo kuu la Utawala. Ametoa pongezi hizo hii leo wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la jengo hilo la kisasa ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75.

Ujenzi huo umetokana na agizo alilolitoa mwezi Agosti 17, mwaka huu, alipotembelea jengo la halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma na kuagiza halmashauri zote nchini kuwa yeyote ambaye imepewa fedha za ujenzi wa Ofisi lakini zitakuwa hazijaanza ujenzi baada ya mwezi mmoja baada ya tarehe hiyo zingenyang'anywa fedha hizo na kupelekwa katika halmashauri ambazo wanaendele na ujenzi.

Akizungumza katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Gairo iliyopo mkoani Morogoro, Mhe.Jafo amesema halmashauri hiyo imekuwa ya mfano kwa kutekeleza maagizo yake.

Amesema halmashauri hiyo imeamua kujichimbia kwenye ujenzi huo kwa kutumia Mkandarasi Pacha Construction Company wa Morogoro ambaye amefanya kazi kubwa na nzuri ndani ya muda mfupi.

Katika hatua nyingine, Mhe.Jafo amekagua ujenzi wa barabara za Gairo mjini huku akimhimiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha anasimamia ujenzi huo ili ifikapo mwaka 2019 ahadi zote alizozitoa Mhe.Rais Dkt.John Pombe Jodeph Magufuli katika barabara za halmashauri hiyo ziwe zimekamilika. Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.5 inajengwa na Mkandarasi C.G.I Contractors LTD.

Akikagua barabara hiyo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya jitihada katika kuhakikisha barabara zinajengwa na kwa kiwango kinachotakiwa na kutoa fedha kwa wakati ili mkandarasi aliyepo aweze kumaliza kazi kama ilivyopangwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Mkandarasi Stephen Aloyce amesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 70 na kuiomba Serikali kukamilisha malipo ya shilingi Bilioni 1.5 ili kumalizia kazi iliyobaki kabla ya kipindi cha mvua kuanza.

Awali akizungumza na watumishi kabla ya kukagua barabara hiyo, Mhe.Jafo amesema kutokana na taarifa ya ukaguzi iliyotolewa ni kwamba halmashauri hiyo ni moja ya halmashauri 6 zilizofanya vibaya katika mfuko wa barabara jambo ambalo linapaswa kusimamiwa vizuri kwa sasa ili lisijirudie tena.

"Taarifa ya ukaguzi inaonyesha Gairo ni moja ya halmashauri 6 zinazofanya vibaya, hili hatutalivumilia, taarifa hiyo ipo nitaiangalia na kama kuna mtu alishiriki katika hilo hata kama hayupo hapa tutamchukulia hatua”, amesisitiza Mhe.Jafo.

Aidha, amewataka kuwa makini na ubora wa barabara zinazojengwa kulingana na thamani halisi ya miradi hiyo ili barabara zinazojengwa zisije kuharibika baada ya muda mfupi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe.Ahmed Shabiby ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi huku akiiomba Serikali kuwasaidia kutatua kero ya maji ambayo bado inawaumiza wananchi wa wilaya ya Gairo.

Mhe.Jafo anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika mikoa mbalimbali na kama sehemu ya utendaji kazi wa kujionea thamani ya shilingi katika miradi hapa nchini kwa lengo la kubaini hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kupima kama miradi hiyo inazingatia ubora unaotakiwa.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.