Serikali Kuendelea kushirikiana na Wadau Kuimarisha Sekta ya Elimu nchini

Na.Fred J.Kibano

Serikali Kuendelea kushirikiana na Wadau Kuimarisha Sekta ya Elimu nchini

Ofisi ya Rais - TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo leo wamekutana mjini Dodoma kufanya Tathmini ya utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (Education Program for Results - EP4R) kwa mwaka 2016/17 ili kuona mafanikio yaliyopatikana, changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kufanikiwa zaidi katika suala la utoaji wa Elimu bora Nchini.

Katika kikao hicho cha siku tatu, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali itahakikisha inatekeleza maazimio yote yaliyofikiwa katika mkutano wa pamoja wa Wadau na washirika wa Maendeleo wa kutathmini Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo uliohitimishwa mjini Dodoma.

Dkt. Akwilapo amesema kupitia mkutano huo na Wadau, wamepata kujadili changamoto zinazoikabili programu katika utekelezaji wa majukumu yake lakini pia imeweza kukubaliana na namna bora ya kuweza kutatua changamoto hizo ili kuweza kuhakikisha programu hiyo inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya Ujifunzaji na Ufundishaji.

“ni jukumu letu kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa ambayo yatasaidia katika kuboresha sekta ya elimu na kufanya elimu ya watoto wetu kuwa bora zaidi”

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa uwazi, kujitoa na kufanya kazi kwa pamoja ili kuwasaidia watoto wa kitanzania kupata elimu bora kwa kuendeleza sekta ya elimu. Lakini pia kuongeza nguvu katika usimamizi wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Halmashauri zote nchini ambalo ni jukumu la Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Bw. Gerald Mweli Mratibu wa Mradi EP4R toka Wizara ya Elimu anasema mpaka sasa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo imeweza kujenga na kukarabati miundombinu chakavu ya shule za Msingi na Sekondari zipatazo 361 katika Halmashauri 129, vyumba vya madarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 4, vyoo 2,832, nyumba za walimu 12, maktaba 4, na uwekaji wa maji katika shule nne (4).

Kwa upande wa vyuo vya Ualimu programu imefanikiwa kukarabati vyuo 10 vya Ualimu ikiwa ni pamoja na kununua vinakilishi 260 vitakavyowezesha walimu kutekeleza majukumu yao kwa urahisi, magodoro 6,730 yatakayotumiwa na wanafunzi pamoja na viti1976 kwa ajili ya wanachuo.

Aidha, programu imenunua vifaa vya maabara 1,696 kwa ajili ya shule za sekondari ambavyo vitasaidia katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na kuongeza uelewa kwa wanafunzi kwa kuwa masomo haya sasa yatafundishwa kwa vitendo, pamoja na kutoa motisha fedha kwa walimu wa shule za msingi na sekodari zipatazo 400 zilizofanya vizuri na zilizoongeza ufaulu katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa mwaka wa 2016 kwa wanafunzi wa Darasa la Saba na Kidato cha Nne.

Kwa upande mwingine Programu imelipa malimbikizo yasiyo ya mishahara ya walimu yapatayo bilioni 32, ununuzi wa magari 54 kwa ajili ya maafisa uthibiti ubora ambayo yatasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao pamoja na ununuzi wa vitabu vya kiada kwa shule za Sekondari.

John Leigh ambaye ni Mtaalamu Elekezi wa Programu amesema katika utekelezaji wa majukumu yao wamefanikiwa kuimarisha Kitengo cha Data naTakwimu cha OR- TAMISEMI kwa kuwapatia mafunzo Wataalamu wa kitengo hicho ili kuboresha utendaji kazi wao.

Progamu hii inatarajiwa kuendelea katika mwaka ujao wa fedha kuanzia mwezi Januari, 2018 baada ya kukamilika kwa awamu hii inayoishia mwezi Desemba, 2017 ambapo Washirika wote watakutana katika kuandaa mwendelezo wake mapema mwezi Desemba, 2017.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.