Serikali yaagiza ukamilishaji Mradi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi Mkoa wa Dodoma

Na.Anjela Msambira

Serikali yaagiza kukamilika mradi jengo la upasuaji Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mhe.Selemani Jafo ameuagiza Uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kufanya tathmini ya uhitaji wa majengo yanayofanana na Makao Makao Makuu ya nchi ili hospitali hiyo iweze kuwa na hadhi ya kimataifa.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Wodi ya wazazi katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuona maendeleo ya ujenzi huo leo Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi hivyo inahitaji kuwa na hospitali inayokidhi vigezo vya kimataifa kwa kuwa na vifaa vya kisasa, majengo imara na kuvutia pamoja na utoaji wa huduma bora kwa jamii.

“Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa sasa ni tegemeo kubwa kwa wananchi ndio maana Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi ili kuhakikisha inapunguza vifo vya wakinamama na watoto pale wanapojifungua jambo ambalo limekuwa ni changamoto katika sekta ya afya” Amesema Mhe. Jafo

Mhe. Jafo amesema ameridhishwa na ujenzi unaoendelea lakini bado hajaridhishwa na miundombinu ya hospitali hiyo kwa kuwa majengo mengi ni chakavu na hayakidhi vigezo vya kuhudumia jamii na kutokuendana na hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Nchi. “Ufike mahali tuje na mabadiliko ya majengo ya hospitali na kuachana na majengo ya kizamani, bali tuweke mikakati ya kujenga majengo ya gorofa ambayo yatachukua nafasi ndogo ya ardhi na kuifanya hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwa ya kisasa na kukidhi mahitaji ya wananchi” Amesema Mhe. Jafo

Amesema kuwa hospitali ya Mkoa wa Dodoma ni kimbilio la wananchi wengi wa mkoa wa Dodoma hivyo inahitaji kuwa na vifaa vya kisasa, majengo mazuri ya ghorofa na mandhari inayovutia ambayo itaakisi uwepo wa Makao Makuu ya Nchi.

Amesema kuwa sababu kubwa ya kuboresha huduma za afya ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na kwa wakati na kukidhi mahitaji ya Serikali kuhamia Dodoma ili kuwasaidia wananchi ambao kimbilio kubwa ni hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Akitoa maelezo ya Mradi wa Jengo la wazazi Meneja Msaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mhandisi Frank Mabubu amesema serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya ujenzi na mpaka sasa zimetumika shilingi billion 3.7 ndani ya miaka tisa ya ujenzi wa jengo hilo.

Ameihakikishia Serikali kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2017 Mkandarasi atakabidhi jengo la wodi ya wazazi kitakachobaki ni uboreshaji wa eneo la nje, ujenzi wa eneo la kupumzikia wagonjwa, ujenzi wa Tanki la maji na ujenzi wa vyoo vya nje ambapo zitahitajika shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi.

Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Bw. James Kihologue ameipongeza Serikali kwa kujenga Wodi ya Wazazi jambo ambalo litapunguza kero kwa wananchi wanaohitaji huduma ya afya na kupunguza vifo vya mama na motto pindi wanapojifungua jambo ambalo litapunguza malalamiko kwa jamii

Aidha, amesema kuwa hakuna upungufu wa watumishi katika hospitali hiyo kwa kuwa waliopo wanasifa na vigezo vinavyohitajika bali changamoto kubwa kwa sasa ni watumishi kutokuwa na maeneo ya kufanyia kazi kutokana na majengo mengi kuwa chakavu.

Serikali iliamua kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi na kupunguza vifo vya mama na watoto, Wodi hiyo inajengwa na kampuni ya PAMCON INTER-CONSTRUCTION LIMITED ya Dodoma na kusimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.