Serikali yakabidhi nyumba za makazi toka iliyokuwa CDA kwa Wakala wa Majengo

Na.Angela Msimbira


Serikali yakabidhi nyumba za CDA kwa Wakala wa Majengo

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe amekabidhi nyumba 141 za iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mjini Dodoma. Akikabidhi nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kwa Wakala wa Majengo Mhandisi Mussa Iyombe amesema nyumba hizo zitakuwa maalum kwa watumishi wenye sifa kulingana na miundo ya kitumishi.

‘’Nyumba ambazo zinakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo ni nyumba za kuishi ambazo awali zilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kuhamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma” Amesema Mhandisi Iyombe.

Mhandisi Iyombe amesema baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa CDA Serikali iliagiza kuwa watumishi wote waliokuwa chini yake kupangiwa kazi kwenye ofisi za Serikali na kipaumbele cha kwanza kilikuwa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuchagua watumishi wanaomfaa kwa ajili ya kuendeleza kazi zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kazi ambayo kwa sasa imekamilika.

Mhandisi Iyombe amesema mali zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka hiyo yakiwemo majengo ya kibiashara kama vile maduka na ofisi zimeelekezwa zibaki chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lakini majengo ya makazi yakabidhiwe kwa Wakala wa Majengo Tanzania(TBA).

‘’Hatuna lengo la kuidhoofisha Manispaa ya Dodoma lakini Serikali inaangalia wanafaidika nini na nyumba hizo wakati majengo yote ya serikali yanatakiwa kuwa chini ya Wakala wa Majengo Tanzania na wakati huo huo watumishi wote wa Serikali wanahamia Dodoma na hawana maeneo ya kuishi na nyumba zipo zilizokuwa zinamilikiwa na CDA zilipangishwa kwa wapangaji ambao hawalipi pango za nyumba kwa wakati” Amesema Iyombe.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Serikali ya kukabidhi nyumba za makazi kwa Wakala wa Majengo Tanzania kwa kuwa Dodoma sasa ni Makao Makuu ya nchi na kumekuwepo na changamoto ya makazi kwa watumishi wanaohamia Dodoma lakini nyumba zinazokabidhiwa zipo katika hali ya matumizi na nyingine zinahitaji ukarabati mkubwa na pia wamezikuta nyumba hizo zikiwa na deni la shilingi bilioni 3 ambazo Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu ilikuwa ikiwadai wapangaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania Msanifu Majengo Elius Mwakalinga amesema kuwa kumekuwepo na tatizo kubwa la upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa Umma hivyo nyumba 438 zitasaidia kupunguza chamngamoto ya upatikanaji wa nyumba hasa kwa watumishi wanaohamia Dodoma.

Amesema kuwa kwa Mkoa wa Dodoma Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ilikuwa na nyumba zaidi ya 400 ambazo zilikuwa kwenye maeneo ya Area D na Kisasa hivyo kwa kupata nyumba hizo sasa watakuwa na nyumba zaidi ya 800 lakini pia Wakala una mpango wa kujenga nyumba 100 mkoani Dodoma mwaka huu na wanatarajia ndani ya miaka miwili kukamilisha ujenzi wa nyumba 500.

Mapema mwaka huu Mhe. Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliivunja Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu na kutokana na utendaji mbovu na kutofikia malengo kwa miaka mingi na kutoa maelekezo kuhusu nini kifanyike baada ya kuvunjwa kwa Taasisi hiyo kongwe.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.