Serikali yaziagiza Halmashauri kukamilisha miundombinu ya shule kwa wakati

Na.Fred.J.Kibano

Serikali yaziagiza Halmashauri kukamilisha miundombinu ya shule kwa wakati

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ametoa agizo kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini ambazo zilipelekewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 16 kwa ajili ya ukarabati, ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na miundombinu mingine ya shule kukamilisha ujenzi na kuhakikisha zinatoa ripoti Ofisi ya Rais TAMISEMI ndani ya miezi mitatu ambapo mwisho wake utakuwa 30/11/2017.

“Naziagiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini ambazo zilipelekewa fedha za ukarabati, ujenzi wa madarasa, miundombinu ya nyumba za walimu na miundo mbinu mingine shule, kwamba ziwe zimekamilisha ujenzi ndani ya miezi mitatu na tarehe ya mwisho ni 30 Novemba, 2017 na ripoti hiyo iwasilishe Ofisi ya Rais TAMISEMI” alisisitiza Mhe. Jafo.

Mhe. Jafo ametoa agizo hilo wakati akifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi Nzasa na Ihumwa nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma ambapo amejionea maendeleo ya ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba 14 vya madarasa na nyumba tatu za walimu katika shule ya msingi Nzasa na kuridhishwa na maendeleo yake pamoja na kuwa na kasoro ndogo ndogo alizoelekeza zirekebishwe. “kama utendaji ulio makini utaendelea ni lazima nchi yetu itaenda mbele”

Aidha, amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma ambaye ni Afisa Elimu wa Manispaa Bw. Mwisungi Kigosi kuongeza idadi ya walimu katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 900 ili kukabilina na upungufu unaojitokeza hususani walimu wapya na wote wanaohamia badala ya kupangwa katikati ya mji wa Dodoma.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Charles Nyaseba amesema shule hiyo ilipatiwa kiasi cha shilingi milioni 252 ambazo zimetumika vizuri katika ujenzi wa miundombinu na hivyo kupelekea kuwa na ziada ya kujenga majengo mengine yanayojengwa na Kikosi Teule Ihumwa kilichopo Dodoma mjini.

Pia katika shule ya msingi Ihumwa Bw. Daudi Mwakalinga amesema jumla ya shilingi milioni 192 zilipelekwa hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2017 na wamekwisha jenga madarasa 9 nje ya yale ya bajeti halisi ya madarasa nane yaliyokusudiwa ambapo mradi umejengwa na Kikosi cha Jeshi Ihumwa. Pia Kikosi hicho cha Jeshi kilitoa msaada wa vyumba viwili vya madarasa ili kupunguza adha ya miundo mbinu ya shule.

Mhe. Jafo amesisitiza kuwa jukumu la Serikali ya awamu ya tano ni kuboresha elimu nchini, “tutafanya uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini. Shule ya Ihumwa inafanya vizuri vizuri Dodoma na hivyo basi iwe miongoni mwa shule kumi bora” alisema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Jafo amejibu baadhi ya maswali ya walimu kuhusu madaraja na madai ya walimu kuwa bado Serikali inamalizia uhakiki wake na baada ya hapo watumishi hao wataweza kupandishwa madaraja lakini pia madeni yasiyo posho za walimu yamelipwa ikiwa ni pamoja na kundelea kulipa kwa awamu madeni mengine.

Amehitimisha ziara yake kwa kuwataka watumishi hao walimu kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili Taifa lisonge mbele kielimu na maendeleo. “Tufanye kazi kwa juhudi na maarifa, kwani nchi yetu inatakiwa kwenda mbele, ni jukumu lenu ninyi nyote mjipange vizuri”

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.