Serikali yazindua Mifumo ya Kielektroniki ya Mipango, Bajeti na Kutolea Taarifa za Afya.

Na Hosseah Nteghenjwa

Serikali yazindua Mifumo ya Kielektroniki ya Mipango Bajeti na Kutoa Taarifa za Afya

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mifumo miwili ya Kielektroniki itakayosaidia kuandaa bajeti kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa na ameonya kwamba mifumo hiyo isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali.

Mifumo iliyozinduliwa ni ya Kupanga Mipango, Kuandaa Bajeti na Kutolea taarifa za hatua za Utekelezaji wa Bajeti (Planning, Budgeting and Reporting System- PlanRep) pamoja na Mfumo wa Kufanya Malipo na Kutoa Taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye Vituo vya Kutoa Huduma (Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).

Akizindua mifumo hiyo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, Mhe.Waziri Mkuu amesema lengo la mifumo hiyo mipya ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi na kamwe isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii.

“Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Viongozi na Watendaji pamoja na Wananchi wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali na isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za Serikali”

Amesema ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa ufasaha ili kuleta tija inayotarajiwa na kila anayehusika ahakikishe anailinda, anaitunza na kuitumia mifumo hiyo ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Pia Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri na Vituo vya kutoa huduma za Elimu na Afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mamlaka zinazohusika kwa wakati.

“Hatutarajii kuona viongozi wa mikoa na halmashauri wakibadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika. Matumizi ya fedha yafanyike kwa kutegemea chanzo cha fedha kilichopokelewa kwa wakati na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika”

Akitoa maelezo ya awali aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George B. Simbachawene amesema mifumo hiyo itaziwezesha Halmashauri kupunguza gharama kubwa katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa Mipango na Bajeti kwani zilikuwa zikitumia muda mrefu na gharama kubwa kwenye kuandaa na kuwasilisha Bajeti.

Hesabu za mwaka 2017/2018 zilizotolewa zinaonyesha kuwa gharama za mchakato wa maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya mwaka kwa Halmashauri 185 ni takriban sh. Bilioni 8.32 za kulipia usafiri (Mafuta), posho ya kujikimu, shajala na gharama za kudurufu Vitabu.

Naye, Kaimu Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Bi. Inmi Patterson amesema mifumo hiyo iliyozinduliwa leo itaisaidia Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uboreshaji wa huduma za jamii lakini pia katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi kwa sababu vinakwamisha utoaji wa huduma mbalimbali za maendeleo kwa jamii.

“Ufisadi ni ugonjwa hatari na unaua kama magonjwa mengine yanavyoua. Ufisadi unazuia maendeleo ya jamii katika nchi husika pamoja na kukwamisha ukuaji wa uchumi na pia unaua ushindani na ndoto za vijana”

Mifumo hiyo iliyozinduliwa imeshirikisha Wizara za Kisekta na Taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency-eGA) kuanzia hatua za awali za ukusanyaji wa mahitaji hadi utengenezaji wa mifumo na ndiyo itakayotumika katika Halmashauri na Vituo vya kutolea Huduma za Jamii.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.