Serikali yaziagiza Halmashauri kuwa na ushirikiano mzuri na Sekta binafsi

Na. Fred J.Kibano

Serikali yaziagiza Halmashauri kuwa na ushirikiano mzuri na Sekta binafsi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mhe. George B. Simbachawene amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi binafsi ambazo zinafanya kazi kwa niaba ya Serikali kama ilivyo kwa shule binafsi hapa nchini ambazo hutoa elimu kwa Watanzania wote sambamba na shule za Serikali ambapo ametoa agizo kwa Halmashauri zote kutobagua walimu wa sekta binafsi.

Akizungumza katika mahafali ya 10 ya shule ya Msingi Martin Luther mjini Dodoma mwishoni mwa wiki amesema anashangazwa kwa baadhi ya Halmashauri kuacha kuwapa fursa za semina, taarifa za chanjo na masuala mbalimbali ambayo mwalimu aliyepo katika shule za Serikali anapatana yule wa shule binafsi anakosa ijapokuwa wana sifa zinazofanana na hivyo kupelekea kuwepo kwa matabaka yasiyo ya lazima na kutaka yaondolewe mara moja.

“Nachukua fursa hii kuagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote kutekeleza wajibu wao kuhakikisha kwamba masuala ya chanjo, taarifa za kielimu na masuala ya semina au kazi mbalimbali zitatolewa kwa wahusika bila kujali kwamba ni shule binafsi au za Serikali”

Amesema ushirikiano baina Serikali na taasisi binafsi ambao kwa hivi sasa changamoto ni mawasiliano ambayo yanakwamisha baadhi ya mambo mfano kutokupata taarifa za masuala ya chanjo ya wanafunzi na maagizo mengine ya kielimu ikiwa ni pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa walimu nchini. “Kama wao ni walimu na wanawafundisha watanzania kwa elimu ile ile, basi nao wanahaki ya kupata huduma hizo za Serikali”, alisisitiza Mhe. Simbachawene.

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene amesema Serikali inatumia kiasi cha shilingi Bilioni 22.25 kugharamia elimu na wazazi wanaposhindwa kuwapeleka wanafunzi katika shule binafsi basi shule hizo ni mbadala wake na zinatoa elimu kwa kiwango kizuri na bila malipo kwani ruzuku yote inatolewa na Serikali lakini pia shule za Serikali zimeboreshwa sana kwa sasa kwani mwaka 2015 wanafunzi bora nchini walitoka katika shule za Serikali.

Aidha, amesema suala la vyeti vya darasa la saba vitatolewa hata kwa wale waliomaliza muda mrefu uliopita ili wawe na kumbu kumbu katika elimu yao na kuhusu Sera ya elimu ambayo ina utaratibu unaoruhusu mihula miwili, mitatu hadi minne ombi lililotolewa katika risala ya wahitimu wa darasa la saba 2017 shuleni hapo, atalizungumza na Wizara ya Elimu ambayo ndiyo inadhamana na utungaji wa sera za elimu nchini ijapokuwa lengo hasa la kuweka mihula miwili lilikuwa kuwapunguzia mzigo wazazi kwa gharama zinazotozwa na shule binafsi.

Akihitimisha hotuba yake wakati wa mahafali hayo amewapongeza wahitimu wa darasa la saba 2017 na kuwatakia mafanikio zaidi mara watakapojiunga na elimu ya sekondari na vyuo mbalimbali vya Serikali na binafsi.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.