Serikali yaagiza asilimia 10 ya fedha za Maendeleo LGDG kutumika kwa maendeleo

Na Fred J. Kibano

Serikali yaagiza asilimia 10 ya fedha za LGDG kutumika kwa maendeleo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe George B. Simbachawene (Mb) ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutumia fedha za Maendeleo za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (LGDG) zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 kiasi cha shilingi bilioni 249 kwa nchi nzima zitumike kwa ajili ya maendeleo ikiwa ni pamoja na asilimia 10 iliyotengwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa Mamlaka hizo.

Akiongea katika ziara yake aliyoifanya mwishoni mwa juma, Mhe. Simbachawene amesema kwa sasa hatuna budi kuangalia maendeleo ya Taifa kwanza na sio kuendelea kulipia mambo yasio ya lazima ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za kujengewa uwezo hali ambayo si sahihi kwa maslai ya Taifa na Serikali ya awamu ya tano.

“Halmashauri zote nchini, zitumie hii fedha ya LGDG (Fedha za Maendeleo za Mamlaka za Serikali za Mitaa), fedha ile ya maendeleo kwa ajili ya maendeleo na si vinginevyo, na maendeleo ninayoagiza kwa Halmashauri zote nchini yawe yanalenga kumaliza maboma yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi kama miradi iliyopita”

Ameyataja mfano wa baadhi ya maboma ambayo yanastahili kutumia fedha hizo yaliyopo wilayani Mpwapwa ni kama madarasa ya shule ya msingi Wangama, Maabara ya Mbuga sekondari, shule ya msingi Shikizi na mengineyo ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mchanganuo wa fedha hizo ambao ni shilingi bilioni 249 asilimia 80 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo, asilimia 10 kwa ajili ya kazi za usimamiaji na asilimia 10 kwa ajili ya kujengewa uwezo ambazo zimekatwa na kuwekwa kwa ajili ya maendeleo.

“Lakini asilimia 10 ambayo inasema ni kujengewa uwezo, ambayo ni watu wanakwenda semina, warsha, mara waite ‘workshop’, hii hapana, hii fedha yote iende kwa ajili ya miradi ya wananchi hasa kwenye maboma. Tunayo maboma mengi sana, hasa sekta ya afya, elimu na mengineyo”

Mhe. Waziri Simbachawene amesisitiza kuwa hata wakati akihitimisha hotuba yake katika bunge la bajeti alitoa kauli ya matumizi ya fedha hizo. “ Nilipokuwa nafunga hotuba yangu kwenye bunge la bajeti nilielekeza asilimia 60 tuipeleke kwenye miradi ya afya na kwa hivyo narudia hapa kusema asilimia inayobaki yote iedne kwenye miradi ya elimu, kasoro ile asilimia 10 usimamiaji kwa sababu ni lazima miradi ili iwe mizuri, lazima isimamiwe” , alisema.

Aidha, amesema Serikali itatoa waraka maalum kuonyesha mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo maalum za maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ndani ya mwaka huu wa fedha wa Serikali.

Mheshimiwa Simbachawene anafanya ziara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hasa maeneo ya vijijini ili kujionea hali halisi ya utendaji, migogoro ya ardhi, utunzaji wa mazingira, huduma kwa wananchi na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ambapo mwishoni mwa wiki ametembelea kata za Mbuga, Kibakwe na Ipera zenye vijiji kadhaa wilayani Mpwapwa kama sehemu ya kazi zake za kujionea maendeleo ya wananchi na kero zao.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.