Serikali yasisitiza kuboreshwa kilimo ili kutoa ajira na kufikia uchumi wa kati

09/08/2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. George Simbachawene amesema kuwa sekta ya kilimo ni eneo muhimu katika kuchangia pato la taifa kwa asilimia kubwa kutokana na kuhusisha watu wengi kwenye uzalishaji wake.

Akifunga kilele cha maonesho ya wakulima nanenane Kanda ya Nyanda za juu kusini katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Mhe. Simbachawene amesema kilimo ni sekta muhimu katika jamii ambapo hutoa ajira ya moja kwa moja kuanzia ngazi ya uzalishaji, uongezaji wa dhamani na wakati wa kuuza bidhaa zake.

Mhe. Simbachawene amesema sekta ya kilimo ndiyo msingi na shabaha ya Serikali katika kuepukana na njaa kwani kupitia sekta ya kilimo inayohusisha idara ya mifugo, Uvuvi, Nyuki, Misitu na Kilimo chenyewe kunapelekea kuondokana na umaskini ili kufikia uchumi wa viwanda.

“Mwaka huu kuna ziada ya chakula kwa asilimia 20 huku Mikoa ya Nyanda za juu kusini ikiwa ndiyo kinara kwa uzalishaji kutokana na fursa ya hali ya hewa nzuri, nguvu kazi na uwepo wa Taasisi mbalimbali zinazochangia kuinua uzalishaji wa kilimo chenye Tija” Amesema .

Aidha ametoa Wito kwa Viongozi kuhamasisha wakulima na wadau wa Kilimo kutumia ardhi kidogo kuzalisha mazao yenye tija kuliko kung’ang’ania maeneo makubwa na kuzalisha mazao kidogo jambo ambalo pia linapelekea uwepo wa migogoro ya ardhi kati ya Wafugaji na wakulima.

Awali akimkaribisha Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema Mikoa ya Nyanda za juu kusini inaiomba Wizara ya Kilimo kutoa nafasi kwa Kanda hiyo kuandaa maonesho ya nanenane 2018 kwa kuwa inayouzoefu wa miaka 25 katika kuandaa na imekuwa na maonesho ya mfano kitaifa.

Amesema malengo ya Kanda ni kuwa na maonesho ya kilimo ya kimataifa hususani Sadc hivyo kupitia maonesho ya Kitaifa kutasaidia kujipima na kujiandaa kwa maonesho ya SADC hivyo Serikali ni vema ikawapa kipaumbele kwa Mikoa ya Nyanda za juu kusini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima wadogo (MVIWATA), Mkoa wa Mbeya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Taifa, Ladislaus Mwanakatwe katika Risala ya Wakulima amesema wakulima wanakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni vipimo kwa wanunuzi wa mazao kwa kuwa hukwepa matumizi ya mizani na badala yake hutumia Lumbesa.

Akifafanua zaidi amesema changamoto nyingine inayowakabili wakulima ni pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakiki wa mazao ya wakulima, bei za mazao kuyumba hivyo kuendelea kutokuwa na uhakika wa maisha bora na kumuinua mkulima mdogo kufikia malengo yake.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.