Serikali Kuhuisha Mfuko wa Maendeleo ya MSM

Serikali Kuhuisha mfuko wa maendeleo ya Serikali za Mitaa
--------------------------------------------------

Serikali imewashukuru Wadau wa Maendeleo kutokana na ufadhili wanaoutoa katika kuchangia jitihada za Serikali katika kuuhisha Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGDG) kwa lengo la kuufanya mfuko huo kuwa bora zaidi wenye kutoa matokeo tarajiwa.

Shukrani hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza na Wadau wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali zinazochangia bajeti ya Serikali katika mkutano uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC). Mhe. Simbachawene amesema Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa una umuhimu mkubwa katika kuinua uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa kwani kupitia mfuko huo miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikiibuliwa na kutekelezwa na wananchi imeweza kukamilishwa na serikali.

“ Mfuko huu ulipoanzishwa wananchi walivutiwa sana na walifanya jitihada za kubuni na kuibua miradi mbalimbali, lakini kuanzia miaka ya 2013 hadi 2015 miradi iliyobuniwa na kutekelezwa na wananchi ilianza kuzorota na ndiyo maana kuna maboma mengi kama vile Vituo vya Afya, Madarasa na Nyumba za Waalimu ambayo hayakukamilika kutokana na mfuko huo kuzorota, lakini sasa kutokana na mfuko huu kuhuishwa miradi hii itakamilishwa.” alisema Mhe. Simbachawene

Mhe. Simbachawene alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeongeza bajeti katika Mfuko huo wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 249 kutoka kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 156 kilichotengwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 . Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imebadilisha mfumo wa upelekaji fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuweka utaratibu wa kuangalia matokeo ya utekelezaji kwa lengo la kuzifanya halmashauri zitimize wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa kodi.

“Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa hakuna mtu yeyote atakayewaletea maendeleo badala yake wao wenyewe wanatakiwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo hatimaye itapewa ushirikiano na serikali katika kuikamilisha, ni vema wananchi watambue kuwa maendeleo yapo katika mikono yao wenyewe.” alifafanua Dkt. Kijaji. Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kufuata kwa vitendo kauli ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Joseph Pombe Magufuli ya kuhakikisha kuwa nchi inafanya bidii ya kujitegemea yenyewe badala ya kutegemea wahisani na hivyo alizitaka halmashauri kufanya juhudi kubwa katika kukusanya mapato ili ziweze kujitegemea zenyewe pasipo kutegemea wadau wa maendeleo.

Naye Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Bw. Lin Zhiyong amesema miradi itakayotekelezwa kupitia mfuko wa LGDG ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha maendeleo ya mikoa na serikali za mitaa yanafikiwa kwakuwa kila mkoa umeonekana kuwa na vipaumbele katika sekta tofauti tofauti.

“Serikali za Mitaa zinapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuvutia wawekezaji, kuongeza fursa za ajira na kuongeza ushuru utokanao na miradi hiyo ili kusaidia Serikali Kuu badala ya kusubiri na kutegemea msaada kutoka Serikali Kuu,” alisema Zhiyong. Wakati huohuo Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara - Mikindani, Bi. Beatrice Dominick amesema kuhuishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa(LGDG) utatoa fursa kwa Halmashauri nchini kukamilisha miradi iliyoachwa viporo.

Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGDG) ulianzishwa na kufanya kazi kuanzia mwaka 2004 hadi 2013 na ulitumika kama njia kuu ya kutekeleza sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D&D) na uliwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutoa huduma kwa wananchi kutokana na mfumo huo kutumika wakati wa kupeleka fedha za maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mfuko huo ulikumbana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wake ambao umepelekea Serikali kuhuisha katika mwaka 2014-2016 ili uweze kutoa matokeo tarajiwa.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.