Waziri Simbachawene Awataka Viongozi Kuzingatia Mipakayao ya Kazi

Na Enock Mhembano.

Waziri Simbachawene Awataka Viongozi kuzingatia Mipaka yao ya kazi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. George Simbachawene amewataka viongozi kuzingatia mipaka yao ya kazi ili kuepusha migongano ya mara kwa mara pamoja na kushirikiana kwa pamoja ili kuwaletea maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Simbachawene ameyasema hayo leo katika ukumbi wa hazina ndogo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi kwaajili ya kuwajengea uwezo Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Wilaya kutoka katika mikoa mitano ya Mara, Simiyu, Mwanza, Geita pamoja na Manyara.

“Sisi Viongozi ni kama timu ya mpira, hivyo ni lazima kila mmoja katika namba yake acheze ipasavyo ili kuleta ushindi, lakini pia pasiwepo na mtu ambaye atacheza kwa kuingilia nafasi ya mwenzie maana kwa kufanya hivyo lazima kutatokea mgongano katika utendaji kazi” Alisema.

Vilevile Mheshimiwa Simbachawene amewataka viongozi hao kwa kupitia mafunzo hayo kwenda kufanya mabadiliko ya kiutendaji kwa kuwa wabunifu ili kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano baina yao wenyewe kwa wenyewe ili kutimiza lengo la pamoja la kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya hayo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Bw. Kadari Singo alizitaja mada ambazo zitatolewa kwa viongozi hao kuwa ni Mbinu za Uongozi, Majukumu na Mipaka ya Kazi, Muundo wa Serikali na namna Serikali inavyofanya kazi, Utunzaji wa Siri za Serikali pamja na Maadili katika Utumishi wa Umma.

Mafunzo hayo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni muendelezo wa mafunzo yanayoendelea kutolewa kwa viongozi na Wakurugenzi hao Tanzania Bara ambayo yanafanyika kwa awamu ambapo hatimaye yatakuwa yamefanyika kwa Wakuu wa Wilaya zote Tanzania Bara.

Ufunguzi huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Musa Iyombe pamoja na Wakurugenzi mbalimbal kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.