Menejimenti ya DCC yapongezwa kwa kurejesha uhai wa shirika

Nuru Juma - MAELEZO

Menejimenti ya DCC yapongezwa kwa kurejesha uhai wa shirika

Serikali imeipongeza Bodi na Menejimenti nzima ya Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) kwa juhudi zao za kurejesha uhai wa Shirika hilo licha ya changamoto wanazo kumbana nazo.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR–TAMISEMI), Mheshimiwa George Simbachawene wakati akipokea taarifa fupi ya Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) na Shirika la Masoko Kariakoo alipokutana na menejinti ya mashirika hayo jana.

Waziri Simbachawene alisema kuwa amepitia taarifa ya Shirika hilo na kuridhika nayo hivyo hana budi kuipongeza timu nzima ya uongozi kwani kwa muda mfupi imeweza kufanya mabadiliko na kuweza kuliinua tena Shirika hilo.

"Pamoja na kuipongeza bodi hii lakini napenda kuwashauri kuangalia maeneo mengine ya kuwekeza kama kufungua maeneo mengi zaidi ya burudani kwani hilo ndilo lilikuwa lengo la kuanzishwa kwa DDC,ikiwa ni pamoja na kuweka mahali ambapo watoto wataweza kucheza ili kuhakikisha shirika linajiongezea kipato na kuiongezea Serikali kipato pia," alisema Waziri Simbachawene.

Mhe. Simbachawene alitumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mashirika ya Masoko Kariakoo na Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanaandaa taarifa nyingine itakayohusisha mali zote za mashirika hayo.

Aidha ameutaka uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo kuwa wabunifu kwa kuanzisha masoko sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi na njia ya kuongeza ajira kwa vijana.

Alilitaka Shirika hilo kuachana na mawazo ya kizamani na badala yake wajipange kimkakati ili kuendana na wakati ikiwemo kufikiria namna ya kuwaza kushusha mizigo katika soko hilo kwani serikali haitaweza kuruhusu malori ya mizigo kufika katika soko hilo ili kupunguza ya kuepuka msongamano katikati ya jiji.

Aliushauri uongozi huo uandae mikakati ya kuwezesha soko hilo kuwa la kiwango cha juu (Super Market) na kuwalipisha wafanyabiashara kiwango kinachoendana na bei halisi ya soko kama ambavyo wapangishaji wengine wamekuwa wakitoza ili kukuza kipato kwa Taifa.

Waziri Simbachawene ameahidi kushirikiana na mashirika hayo katika kutatua changamoto ambazo zinahitaji msaada wa uongozi na kuwataka wafanye kazi kwa bidii kwani Serikali ya Awamu ya Tano inahitaji watu wanaojituma na kuchapa kazi.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam Meneja Mkuu wa Shirika hilo Rwandiko Manumbu alisema kuwa pamoja na changamoto wanazokumbana nazo Shirika limefanikiwa kutoa shilingi milioni 140/- kama gawio kwa mwanahisa wake ambaye ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

"Mhe. Waziri, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Shirika hili tumeweza kutoa gawio la kiasi cha shilingi milioni 140/- kwa Halmashauri ya Jiji na haya ni mafanikio makubwa kwetu," alisema Manumbu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amempongeza Waziri Simbachawene kwa utayari wake wa kushughulikia changamoto zinazo yakabli mashirika hayo ikiwa ni pamoja na kutenga muda wake kuja kusikiliza matatizo yao.

Pamoja na pongezi hizo Mwita alishauri Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) kuangalia uwezekano wa kurejesha bendi za muziki kama ambavyo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyokuwa amedhamiria wakati wa uanzishwaji wa Shirika hili.

Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) na Shirika la Masoko Kariakoo ni mashirika ya Umma yanayoongozwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Sheria za Makampuni namba 2012 ya mwaka 1971 na Sheria ya Bunge namba 36 ya mwaka 1974, 'The Kariakoo Market Corporation Act, 1974'

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.