Halmashauri za miji 18 nchini zapongezwa kwa kutekeleza vizuri mradi wa ULGSP

Halmashauri za miji 18 nchini zapongezwa kwa kutekeleza vizuri mradi wa ULGSP

Serikali imezipongeza halmashauri 18 zinazotekeleza Mradi wa kuimarisha halmashauri za Manispaa na miji (ULGSP) Tanzania bara kwa kutekeleza vizuri mradi huo katika halmashauri zao.

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 5 aprili, 2017 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Utawala bwana Mohamed Pawaga wakati akifungua kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu alisema katika mwaka wa nne wa utekelezaji wake mradi wa kuimarisha halmashauri za miji umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, mifumo ya upangaji miji, ongezeko la makusanyo ya vyanzo vya mapato hususani kodi ya majengo, na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ya halmashauri hizo.

"Sote ni mashuhuda kwa namna mradi huu ulivyoboresha maendeleo ya miundombinu katika miji yote inayotekeleza mradi huu hasa ujenzi wa barabara, masoko, vituo vikuu vya mabasi, uboreshaji wa mifumo ya majisafi na majitaka katika miji hiyo," alisema Katibu Mkuu.

Pia Katibu Mkuu amepongeza utekelezaji wa mradi huo kwa kutoa kipaumbele kwenye eneo la mazingira ambalo limekuwa likisahauliwa mara nyingi katika miji.

Ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo unaongeza ufanisi katika utekelezaji wa mradi wa kuimarisha halmashauri za miji, serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI itahakikisha kuwa inaendelea kuweka mazingira mazuri ikiwemo kuhakikisha kuwa matatizo yote yanayojitokeza katika utekelezaji wake yanatatuliwa kwa haraka na kwamba halmashauri za miji na sekretarieti za mikoa zinatoa msaadaa wa kutosha kwa halmashauri.

Kwa upande wake Mtaalamu Mwandamizi anayehusika na maendeleo ya miji na kukabiliana na majanga kutoka Benki ya Dunia bwana Eric Dickson aliwataka watendaji wa serikali kutoka halmashauri zinazotekeleza mradi huo kwenda kujifunza katika halmashauri nyingine zilizofanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa mradi ili kuboresha utendaji katika miji yao.

Alitolea mfano wa Manispaa za Morogoro na Moshi kama miji ya mfano katika utekeleza wa mradi huo na kwamba halmashauri nyingine zinapaswa kutembelea miji hiyo ili kuona namna zilivyotekeleza kwa mafanikio.

Aliongeza kuwa nchi za Ethiopia na Uganda zimekuwa zikifuatilia utekelezaji wa mradi huu na zimekuwa zikifanya mawasiliano na ofisi yake ili kuja kujifunza namna mradi huu ulivyotekelezwa kwa mafanikio nchini.

Naye Mratibu Msaidizi wa Mradi wa ULGSP Mhandisi Gilbert Mfinanga alisema kuwa katika mwaka 2016/17 halmashauri zinazotekeleza mradi huu zimepokea jumla ya shilingi 94,747,030,473 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema kuwa mradi wa ULGSP ni mradi wa matokeo ambapo kila halmashauri inyoutekeleza hupimwa kila mwaka kupitia vigezo na viashiria mbalimbali vinavyotumika kupima matokeo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizokusudiwa na matokeo haya yanatumika kukokotoa kiasi cha fedha kitakachotolewa kwa kila halmashauri.

Mradi huu unatekelezwa katika Manispaa za Morogoro, Singida, Shinyanga, Musoma, Tabora, Bukoba, Moshi, Lindi, Songea, Iringa na Sumbawanga. Pia mradi huo unatekelezwa katika halmashauri za miji ya Geita, Bariadi, Babati, Korogwe, Kibaha, Njombe na Mpanda.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.