Dkt Chaula ataka wanawake wawe chachu katika maendeleo ya Viwanda

Na Sylvia Hyera

Dkt Chaula ataka wanawake wawe chachu katika maendeleo ya Viwanda

Naibu Katibu Mkuu Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Dkt Zainabu Chaula amewataka wanawake nchini kuwa chachu katika maendeleo ya Viwanda ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika familia.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani iliyofanyika katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili Cheshire, kilichopo Miyuji nje kidogo ya Mji wa Dodoma, Dkt. Chaula aliwataka wanawake kuanzisha na kujiunga katika vikundi vidogovidogo vilivyosajiliwa ili kupata fedha ambazo zitawawezesha kuwekeza katika viwanda hivyo.

"Tanzania katika kuelekea uchumi wa kati kupitia viwanda, wanawake tujitokeze, tuwajibike na tusirudi nyuma tuwekeze katika viwanda vidogo vidogo ili kuchangia na kuinua kipato cha familia zetu," alisema Dkt. Chaula.

Aidha Naibu Katibu Mkuu alisema pamoja na kuwa wanawake wanaweza lazima nidhamu iwepo majumbani.

"Wanawake ni nguzo ya amani katika familia, hakuna mbabe katika ndoa, wanatakiwa kusimamia hata watoto wawe na misingi na maadili mazuri bila amani na upendo familia inakuwa haijasimama," alisema

Dkt Chaula ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, na wanawake kutoka taasisi mbalimbali zilizopo wilaya ya Dodoma mjini, walikitembelea kituo cha Cheshire na kutoa misaada yenye thamani ya shilingi 3,723,000.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bibi Christina Mndeme aliwataka wanawake kuungana pamoja kupiga vita ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia na kuhahakisha wanatoa malezi bora katika familia ili kuleta maendeleo na amani nchini.

Bibi Mndeme alisema kila mmoja ana jukumu la kupambana na mimba za utotoni.

"Leo kwenye shule za sekondari mimba ziko 72 na shule za msingi mimba sita, kinamama tunajua mtoto wa darasa la nne akipewa ujauzito atajifunguaje?" alihoji mkuu huyo wa wilaya.

Alisema wazazi na walezi kuongea na mabinti zao pamoja na jamii kusaidia kupiga vita ukatili wa kijinsia kwani vimekuwa nyingi na kumekuwa na matukio mengi ya ubakaji na ulawiti.

"Kinamama wasimamie malezi katika familia ukiona mtu anamsogelea binti kuwa mkali," alisema.

Alisema ukatili wa kijinsia umekuwa ukirudisha nyuma uchumi wa nchi unadhalilisha wanawake na kutaka watoto waambiwe waache tamaa ili wafikie ndoto zao.

Akitoa shukrani kwa misaada iliyotolewa kituoni hapo Sista Valentina Baidu ambaye ni Mwalimu wa elimu maalum na Mkuu wa kituo hicho ameiomba Serikali na wadau mbalimbali wa elimu kusaidia kituo hiko kwani kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa walimu 3, ukarabati wa miundombinu na huduma ya maji kutoka DUWASA.

Kituo cha Cheshire kilichopo Miyuji Mjini Dodoma kilianzishwa mwaka 1987 kwa ushirikiano wa Serikali na Jimbo kuu la Kanisa Katoliki Dodoma kinapokea watoto wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 10 na kuwapa elimu na makuzi ya awali kwa watoto wenye matatizo ya kiakili ,kituo hiko kina jumla ya watoto 40 na walimu wanne.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.