Wakuu wa Mikoa na Wilaya waaswa kuzitumia taasisi za maadili

Na Sylvia Hyera

Wakuu wa Mikoa na Wilaya waaswa kuzitumia taasisi za maadili

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia busara na hekima wanapowawajibisha watendaji walio chini yao.

Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 06/03/2017 mjini Dodoma, Mhe.Simbachawene amesema Wakuu wa Mikoa na Wilaya kabla ya kuchukua hatua dhidi ya watendaji wanapaswa kujua matatizo yaliyopo kwa undani na wakishayajua watumie busara ya namna ya kuyashughulikia.

"Malalamiko ya kiutendaji yapo mengi sana lakini jambo muhimu la kuzingatia kwamba mtendaji awekwe ndani pale ambapo uwepo wake nje unahatarisha hali ya usalama wa mali au wananchi kwa muda ule," alisema.

Amesema kuwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa ana uwezo wa kumuweka ndani kwa mujibu wa sheria wakati taratibu nyingine za kinidhamu zinafuatwa.

Mhe.Waziri alisema kuwa watumishi wa Serikali wana vyombo vyao ambavyo vinashughulika na maadili ya watumishi wa Umma katika utendaji kazi wao, hivyo kama viongozi katika Mamlaka za Wilaya na Mikoa waone kuwa watendaji wanaweza kuchukuliwa hatua na kuwajibishwa kupitia vyombo hivyo vya maadili.

Pia aliongeza kuwa viongozi wanapompa adhabu mtendaji wa Serikali wanatekeleza kwa mujibu wa sheria ila wanatakiwa wachukue hatua kwa lengo la kumuwajibisha na sio kufanya kwa kisasi au sababu binafsi , Mkuu wa Mkoa atamuweka ndani Mtendaji kwa masaa 48 na Mkuu wa Wilaya atamuweka ndani Mtendaji wa muda wa masaa 24 .

Wakati huo huo, Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Shirika Elimu Kibaha Dkt. Cypirian Mpemba ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za kiutendaji zinazolikabili shirika hilo.

Mhe. Simbachawene alifafanua kuwa kumekuwepo malalamiko dhidi ya Mtendaji Mkuu wa wa shirika la Elimu Kibaha ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI iliunda kikosi kazi ili kufanya uchunguzi dhidi ya malalamiko hayo na kugundua kuwepo kwa changamoto katika uendeshaji wa Shirika hilo.

Alisema uamuzi wa kumsimamisha Dkt. Mpemba umechukuliwa kwa kuwa tuhuma na malalamiko mengi ya awali yaliyojitokeza dhidi yake yanajenga hoja ya kuhitajika kufanyika kwa uchunguzi zaidi ambapo kwa sasa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha inakaimiwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.