Wilaya ya Chamwino yapewa mwezi mmoja kukamilisha mradi

Na Mathew Kwembe

Wilaya ya Chamwino yapewa mwezi mmoja kukamilisha mradi

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo ameipa mwezi mmoja halmashauri ya Wilaya ya Chamwino iliyopo mkoani Dodoma kuhakikisha kuwa inakamilisha mradi wa maji.

Akizungumza na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo na wananchi wakati akikagua mradi huo wa maji katika kijiji cha Wilunze tarehe 06/03/2017, Mhe.Jafo aliitaka halmashauri hiyo kumsimamia mkandarasi huyo ili wananchi wa kijiji hicho wapate maji.

Mbali na hilo, pia ameagiza Halmashauri hiyo kuzuia fedha ya mkandarasi iliyosalia kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka ubora wa mradi huo utakapoonekana.

Hata hivyo alisema mkandarasi aitwaye M/s Kijima fedha aliyopewa hadi sasa haiendani na kazi iliyofanyika huku akitilia mashaka mabomba yaliyowekwa kwamba yapo chini ya kiwango.

"Hadi sasa mkandarasi umepewa Sh. Milioni 305.7, gharama ya mradi kwa ujumla ni Sh.Milioni 347.9, umebakisha fedha kidogo ambayo ni Sh.milioni 42.1 tukiangalia kazi iliyofanyika hata haiendani na fedha ulizopewa, unachokifanya hapa ni kama maigizo huu mradi haujafikia asilimia 90 na haya mabomba yanaonekana yapo chini ya kiwango maana yameanza kupasuka," alisema Mhe.Jafo

Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri alimtaka Mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo na kwamba ifikapo Aprili 3, mwaka huu atarudi kukagua na kuiagiza serikali ya wilaya hiyo kuwakamata watu watakaoharibu miundombinu ya maji.

Aidha alisema katika miradi mingi ya maji aliyotembelea amekutana na changamoto ya wakandarasi kuweka mabomba ambayo yapo chini ya kiwango na kusababisha wananchi wanapokabidhiwa mradi kushindwa kuiendesha.

Naye, Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Camp A, Waziri Sengoli, alisema wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakipata adha ya maji ka takriban miaka saba huku akiwaumbua viongozi wa Halmashauri hiyo kwamba wamekuwa hawatembelei kukagua mradi huo.

"Sisi kama wajumbe wa serikali ya kijiji tumekuwa tukihoji lakini tunaambiwa hatuna mamlaka, hivi hizi koki unazoziona zimefungwa usiku baada ya kusikia unakuja," alisema

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Athuman Masasi, alikiri kuwa kuwa walifunga koki hizo usiku na kwamba katika Halmashauri hiyo ipo changamoto ya kiutendaji.

Kwa upande wake, Mkandarasi huyo Enock Masanja, alijitetea kuwa ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati kutokana na kutopata fedha kwa wakati huku akiahidi kwa muda aliopewa na Waziri Jafo ataweza kukamilisha na wananchi watapata huduma ya maji.

Ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2013 na kudai kuwa utekelezaji wake umesuasua hali inayosababisha wananchi wa eneo hilo waendelee kupata adha ya maji.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.