Serikali yawaonya Wauguzi wanaowanyanyasa Wajawazito

Na.Fred Kibano

Serikali yawaonya Wauguzi wanaowanyanyasa Wajawazito

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewaonya wauguzi kuacha kutoa lugha chafu kwa wagonjwa hasa akina mama wanaokwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya ya Kongwa.

Mhe.Jafo ametoa onyo hilo alipofanya ziara ya kushtukiza wilayani Kongwa ili kujionea changamoto zinazowakabili wagonjwa na kuusisitizia uongozi wa hospitali hiyo kuwa makini na kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wagonjwa ikiwemo kushughulikia kero nyingine za hospitali hiyo.

"Nimepokea malalamiko ofisini kwangu kuhusu kauli za baadhi ya wahudumu kwenye hospitali yako (Mganga Mkuu wa Wilaya, DMO) siyo nzuri, inafikia hatua baadhi ya watu wanapoteza watoto wao hapa hapa," alisema.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dkt Festo Mapunda amesema amekwisha kaa kikao na wauguzi wa hospitali hiyo na kukemea vikali tabia hiyo ambapo ameanzisha dirisha la malalamiko na kutoa namba zake za simu.

Wakati huo huo Mhe. Jafo ameongea na watumishi, wakuu wa Idara na Madiwani ambapo aliwataka kuwajibika katika suala la utunzaji wa vyanzo vya maji unaosababisha uhaba wa maji katika wilaya hiyo kwani katika chanzo kikuu cha maji kilichopo mlima mongo watu wamelima hadi mlimani na kusambaratisha msitu wote.

"Maji yaliyokuwa yakija Chamkoroma yanakuja Suguta hadi Mang’weta lakini sasa hali si hivyo, maji yamekauka vyanzo vyote vya maji watu wamefyeka na maafisa wapo. Tunazungumza sasa inawezekana miaka kumi ijayo hali ikawa mbaya zaidi ya sasa," alisisitiza Mhe. Jafo.

Kwa upande wake Mhandisi wa maji wilaya Bwana Salim Bwaya amesema upatikanaji wa maji ni wastani wa asilimia 47.5 na ni kwa mgao kutokana na kuwepo kwa vyanzo ambavyo havitoshelezi kwa wakazi wa wilaya hiyo kongwe nchini.

Mhe. Jafo amehitimisha ziara yake kwa kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja lililopo katika kijiji cha Sejeli kinachounganisha kijiji cha Matuge na wilaya ya Kiteto ambao unafanywa na kampuni ya Rafiki Building Contractors Company Limited ya Morogoro ambapo ameridhishwa na hali ya ujenzi wa daraja hilo unaokadiriwa kufikia asilimia 75.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa Bwana Ngusa Izengo ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na watendaji wake na watumishi wote na kuhakikisha hawafanyi kazi kwa mazoea.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.