Manispaa ya Dodoma yatakiwa kuzuia uuzaji bidhaa pembeni ya barabara

Na. Sylvia Hyera

Manispaa ya Dodoma yatakiwa kuzuia uuzaji bidhaa pembeni ya barabara

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa Mhe. Selemani Jafo amemtaka Mkurugenzi wa Manspaa ya Dodoma Bw. Godwine Kunambi kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa soko kuu la Majengo lililopo mjini Dodoma kutoweka bidhaa zao pembezoni mwa barabara iliyopo kando ya Soko hilo.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo aliridhishwa na maendeleo yake na kukiri kuwa ujenzi upo katika hatua nzuri tofauti na alipotembelea hapo awali.

"Barabara ipo katika hatua nzuri nimefarijika lakini japo na uzuri wake kuna kasumba ya wafanyabiashara kuweka bidhaa pembezoni mwa barabara mwisho wa siku thamani ya barabara hii inashuka, hakikisha makusudio ya ujenzi yapo pale pale ,hatutarajii watu waweke bidhaa barabarani," alisema na kuongeza kuwa barabara hiyo inapaswa kubaki katika hali yake ya kawaida na itumike kwa matumizi yaliyotarajiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bwana Kunambi amesema hatawaruhusu watu kutumia barabara kwa matumizi yasiyokusudiwa na atahakikisha kuwa usafi wa hali ya juu unazingatiwa.

Aidha bwana Kunambi ametoa siku saba kwa watu wanaofanya biashara zao kandokando ya barabara ya jamatini hadi stendi kuu ya mkoa nyakati za jioni kuhakikisha kuwa hawafanyi biashara zao katika maeneo hayo kwani wanahatarisha maisha yao na afya za watu wengine. "Wananchi watumie masoko yaliyopo kama soko la matunda Tambuka reli, tutachukua hatua dhidi ya watakaokaidi sheria na tutaendelea kupokea maagizo ya Viongozi wetu Serikalini."

Pia Naibu Waziri alitembelea dampo lililopo katika kijiji cha Ntyuka nje kidogo ya manispaa ya Dodoma kukagua ujenzi wa dampo ambapo ameridhishwa na taarifa na maendeleo ya ujenzi huo na kumuagiza mkurugenzi wa Manispaa kuweka mikakati ili kuhakikisha kutowepo kwa makazi ya watu wavamizi maeneo ya dampo kama ilivyo katika miji mingine nchini.

Mhe. Jafo alisema lengo ni kuwa na miradi hiyo mikubwa nchi nzima ila kuna tabia ya watu kuanzisha makazi pembezoni au karibu na maeneo ya dampo bila kujali kuwa wanahatarisha afya zao hivyo alimtaka mkurugenzi afanye mikakati ya kuweka mipaka ya eneo kuonyesha mwisho wa makazi ya watu sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.

"Lazima tuhakikishe tunalinda eneo linalozunguka dampo hili na kutoa elimu kwa wananchi ili wawe na weledi mzuri wa matumizi ya dampo ,kuzuia uharibifu wa mitambo iliyopo na kulinda afya zao kwa ujumla," Alisema Mhe. Jafo

Kwa upande wake, Mhandisi wa Manispaa ya Dodoma, John Nchila alisema kuwa baada ya miaka sita au saba taka za dampo hilo zitaweza kuzalisha gesi ambayo itatumika kwa matumizi ya nishati , aliongeza kuwa kutokana na ujio wa makao makuu mradi huo umeongezewa mashimo mawili ya ziada na kuweka jumla ya mashimo matatu ili kukidhi haja ya kuifadhi taka ambapo mradi utatumia jumla ya shilingi bilioni saba hadi mwisho wa ujenzi huo ifikapo juni, 2017.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.