Mikoa 10 yajengewa uwezo katika usimamizi wa fedha za umma

Na. Mathew Kwembe

Mikoa 10 yajengewa uwezo katika usimamizi wa fedha za umma

Serikali imepokea shilingi bilioni 5.2 kutoka Shirika la Misaada la Uingereza DFID kwa ajili ya kuijengea uwezo wa usimamizi wa fedha mikoa 10 nchini ili iweze kuzisaidia Halmashauri zake katika kuboresha masuala muhimu yanayohusu usimamizi wa fedha za umma.

Akifungua kikao cha kamati tendaji kinachojadili utekelezaji wa shughuli za programu za kipindi cha robo mwaka kinachoishia 2015/16 cha Watendaji wa mikoa wanaoshiriki katika usimamizi wa fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa jana mkoani Mtwara, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bwana Bernard Makali alisema kiasi hicho ni kati ya shilingi bilioni 17 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo ya miaka mitano ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2012/2013 na unatarajia kukamilika mwaka 2016/2017.

Alisema fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kuzijengea uwezo sekretarieti za mikoa na taasisi nyingine za serikali zinazoshiriki programu hiyo kama vile wizara ya fedha na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kutoa mafunzo na matumizi ya mifumo ya usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele na Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha ni pamoja na kutoa mafunzo na matumizi ya mifumo ya usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo mifumo ya ukusanyaji mapato na mifumo ya utoaji wa taarifa za fedha (EPICOR), matumizi ya fedha na uwajibikaji ikiwemo udhibiti wa masuala ya rushwa," alisema bwana Makali

Alisema kuanzishwa kwa programu hiyo kumeisaidia mikoa hiyo 10 inayotekeleza programu hiyo kupunguza idadi ya halmashauri zinazofanya vibaya katika masuala ya usimamizi wa fedha ikiwemo kupungua kwa hati chafu.

Alisema ingawa katika mwaka 2014/15 kulikuwa na halmashauri zilizoongezeka na kupata hati zenye mashaka kutokana na sababu ya kutotenganisha tathmini ya majengo na ardhi lakini mikoa imejipanga kufanya maboresho katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa programu na kuhakikisha kuwa halmashauri zinarejea tena kwa kuwa na hati safi.

Bwana Makali alisema kutokana na programu hiyo kutekelezwa kwa mafanikio makubwa, washirika wengine wa maendeleo mbali na DFID wameonyesha nia yao ya kusaidia utekelezaji wa programu hiyo katika awamu ya tano ya programu ya maboresho ya fedha ambapo katika awamu hiyo serikali inakusudia kuishirikisha mikoa yote 26 ya Tanzania.

Kwa mujibu wa bwana Makali, katika utekelezaji wa awamu ya sasa Serikali iliweka vigezo na kushirikisha mikoa 10 kutekeleza programu hiyo, kwa kuijumuisha mikoa yenye halmashauri zilizofanya vizuri, na zilizofanya vibaya katika usimamizi wa fedha za umma kama ilivyoripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nakuhusisha mikoa mipya.

"Tumeijumuisha mikoa iliyofanya vizuri katika programu hii ili iweze kuifundisha namna ya kukabiliana na changamoto mikoa ambayo haikufanya vizuri lakini pia kuelezea uzoefu wake kwa mikoa mipya ambayo ilianzishwa hivi karibuni," alisema.

Mapema Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Usimamizi wa fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi bwana Shomary Mukhandi alieleza malengo ya kikao hicho kuwa ni kupokea na kuchambua taarifa za utekelezaji wa shughuli za programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika mikoa 10 inayotekeleza programu hiyo pamoja na ofisi ya Rais TAMISEMI.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma (PFMRP IV) katika Ofisi ya Rais TAMISEMI bibi Upendo Mangali, utekelezaji wa programu hii unahusisha mikoa 10 na ulianza mwaka 2012/13 na ni programu ya muda wa miaka mitano ambayo inakamilishwa mwaka 2016/17.

Bibi Mangali aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Mara, Mtwara, Simiyu, Katavi, Geita, Rukwa, Kigoma, Ruvuma na Njombe

Alisema kuwa programu hii inatekelezwa kwa kushirikiana na wataalamu washauri (wazawa) ambao wapo katika ngazi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, na mikoa 10 ili kusaidia na kushauri utekelezaji sahihi wa shughuli za programu.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.