Serikali yapiga marufuku Kilimo na Ufugaji bwawa la Cholesamvula

Na. Mathew Kwembe

Serikali yapiga marufuku Kilimo na Ufugaji bwawa la Cholesamvula

Serikali imepiga marufuku shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo lote linalozunguuka milima ya Cholesamvula wilayani Kisarawe ili kuepusha uharibifu wa mazingira na kusababisha mmomonyoko wa udongo kutoathiri mradi mkubwa wa bwawa la maji linaloendelea kujengwa kijijini hapo.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa bwawa hilo juzi ambalo limeigharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 1.5, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo alisema kuwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe uhakikishe kuwa shughuli za kilimo na ufugaji hazifanyiki katika eneo hilo ili kuepusha uharibifu wa mazingira na mmomonyoko wa ardhi utakaosababisha bwawa hilo kujaa udongo pindi mvua ikinyesha.

Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa Halmashauri kupiga marufuku shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo hilo na maeneo yote ya vyanzo vya maji ili kulinda hifadhi ya mazingira lakini pia kuzuia mmomonyoko wa udongo utakaosababisha udongo kujaza bwawa hilo.

"Halmashauri hakikisheni mnazuia shughuli za kilimo na ufugaji karibu na bwawa hili kwani tukiruhusu tu pindi mvua ikinyesha udongo utalijaza bwawa hili kwani ardhi itakuwa wazi," alisema Naibu Waziri na kuongeza kuwa halmashauri inatumia kila mbinu kuhakikisha kuwa inayaondoa majani yaliyo ndani ya bwawa hilo mapema iwezekanavyo kabla ya mvua kuanza kunyesha.

"Hakikisheni kuwa mnayaondoa majani na miti iliyopo ndani ya eneo la bwawa kabla ya mvua kuanza kunyesha, tukichelewa kuyaondoa majani na miti pindi bwawa hili litakapojaa maji tutashindwa kuyatumia maji haya kwani majani na miti itaoza na kuharibu maji ya bwawa," alisema.

Aidha Naibu Waziri Jafo amepiga marufuku bwawa hilo kutumiwa na mifugo na badala yake ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kutenga eneo maalum mbali na bwawa hilo kwa ajili ya kutumiwa na mifugo.

Naibu Waziri alisema kuwa ni jukumu la halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kuhakikisha kuwa inalitunza bwawa hilo na vyanzo vyake vya maji kwani serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha bwawa hilo.

Kwa upande wake Mhandisi wa Maji wilaya ya Kisarawe Majid Mtili alisema kuwa bwawa hilo litakakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji yenye mita za ujazo milioni moja na kwamba hadi sasa asilimia 72 ya ujenzi wa bwawa imekamilika.

Awali Mhandisi Mshauri Said Ganga wa kampuni ya Inter Consult LTD alimweleza Naibu Waziri shughuli zilizokwishafanyika katika ujenzi wa bwawa hilo na kumuomba asaidie kuharakishwa kwa zoezi la kuondolewa kwa majini na miti katika bwawa hilo kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua.

Bwawa hilo litatumiwa na wakazi wa vijiji vya Cholesamvula, na Kwala, na pia wakazi wa Panga la Mwingereza na Mtinani watafaidika na maji ya bwawa hilo.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.