Mhandisi Manispaa ya Kinondoni apewa siku 60 kukamilisha ujenzi wa madarasa

Na. Mathew Kwembe

Mhandisi Manispaa ya Kinondoni apewa siku 60 kukamilisha ujenzi wa madarasa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR TAMISEMI), Mheshimiwa George Simbachawene, amempa siku 60 Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, Brighton Kimaro, kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa madarasa mawili, matundu nane ya vyoo, nyumba sita za walimu na tenki moja la maji.

Mheshimiwa Simbachawene alitoa agizo hilo, baada ya kutembelea eneo la ujenzi katika Shule ya Sekondari Matosa, kata ya Goba wilaya Ubungo na kukuta msingi wa majengo ya madarasa mawili ukiwa umeishia kwenye hatua ya uchimbaji licha ya kupatiwa Sh. milioni 50 kutoka serikali kuu na Sh. milioni 15 kutoka halmashauri kwa ajili ya kazi hiyo.

Akizungumza na watendaji wa wilaya ya Ubungo katika Shule ya Sekondari ya Matosa, wakati wa ziara yake ya kukagua Shule za Jiji la Dar es Salaam, zilizonufaika na utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Shule ya Sekondari (MMES) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa asilimia 30, Mheshimiwa Simbachawene alisema, amesikitishwa na uzembe huo wa Mhandisi wa manispaa.

"Sikubaliani na maelezo yako na siko tayari kukufukuza kazi ingawa kuna dalili za kuondoka na mtu hapa, ila nakupa siku 60 hadi Desemba 30 mwaka huu, ujenzi uwe umekamilika nataka nikipita hapa wakati naelekea Dodoma nikute mmeshaanza kazi, nikute msingi hapa na ujenzi wake uanze haraka iwezekanavyo," alisema.

Awali Waziri Simbachawene alielezwa kuwa mradi huo, ulishindwa kuanza kwa wakati licha ya serikali kutoa fedha tangu mwezi Mei mwaka huu, kwa sababu hali ya mazingira na udogo uliopo eneo la ujenzi (aina ya ufinyazi) si rafiki kwa ajili ya kujenga.

Akielezea mradi wa ujenzi huo, Mhandisi Kimaro, alimueleza Mheshimiwa Waziri kuwa, walimpata mkandarasi wa kujenga eneo hilo lakini mara baada ya kuchimba msingi alibaini udongo huo hauwezi kuhimili ujenzi na hivyo kuamua kusitisha kazi hiyo hadi hapo watakapofanya utafiti wa kitaalam kabla ya kuendelea.

Naye Afisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni, Rodgers Shemwelakule,alimueleza Waziri Simbachawene kuwa, halmashauri ilipeleka fedha Sh. milioni 15 kwa ajili ya kuchimba udongo huo ili kazi ya ujenzi wa madarasa na majengo ya nyumba za walimu uanze lakini hakuelewa sababu za kuendelea kusuasua kwa mradi huo.

Mbali na hilo, Mheshimiwa Simbachawene, alieleza kusikitishwa kwake na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu na viongozi wa Shule za Sekondari nchini wenye lengo la kuifanya serikali ichukiwe kwa kukataa kufanya mahafali ya kidato cha nne kwa madai serikali imekataza.

Alisema wazazi na walimu alipaswa kushirikishana na kueleza viongozi wa Serikali na kuchangishana fedha kwa ajili ya mahafali kwa sababu serikali haina jukumu la kuchangia fedha hizo, isipokuwa walitakiwa kuomba kibali kwa Mkuu wa Mkoa na kufanya shughuli hiyo chini ya kamati ya shule.

Pia aliwataka wazazi, walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Matosa, kutimiza wajibu wao ili shule hiyo ifaulishe wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.