Naibu Waziri ataka madarasa shule ya msingi yakarabatiwe

Na. Nasra Mwangamilo

Naibu Waziri ataka madarasa shule ya msingi yakarabatiwe

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuhakikisha unakamilisha ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Chang’ombe, ifikapo tarehe 10 Januari, 2017 kabla ya msimu wa masomo kuanza.

Mhe. Jafo alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imetoa jumla ya shilingi Milioni 192 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na ukarabati wa majengo machakavu katika shule ya msingi Chang'ombe na kuwataka watendaji hao kutumia vizuri fedha hizo zilizotolewa na serikali.

Mhe. Jafo alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kata ya Chang'ombe ambapo katika ziara hiyo alibaini changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo zikiwemo upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo.

"Natoa agizo kwa Afisa Mipango na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa, ifikapo tarehe 10 Januari, 2017, ujenzi wa majengo haya uwe umeshakamilika na muhakikishe shule yote inakuwa mpya," alisisitiza Mhe. Jafo na kuongeza kuwa angependa kazi hiyo ifanyike ndani ya muda na kutojengwa chini ya kiwango cha ubora.

Aidha, Naibu Waziri Jafo alionyesha kutoridhishwa na taarifa za ujenzi wa zahanati ya kata ya Chang'ombe ambayo taarifa zilizotolewa zilionyesha kuwa hazikuwa sahihi ukilinganisha na idadi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.

"Sijaridhishwa kabisa na ujenzi unaoendelea katika zahanati hii na siamini kama kulikua na usimamizi mzuri, nataka niletewe taarifa inayoambatana na taarifa ya mkandarasi aliyehusika na ujenzi pamoja na mchakato wa manunuzi ya vifaa na maendeleo ya ujenzi ili nijiridhishe na suala hili," aliagiza Naibu Waziri Jafo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Jafo alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa Manispaa ya Dodoma na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia umuhimu wa mahitaji ya wananchi na kuyawekea kipaumbele mambo ya msingi ikiwamo huduma za afya na elimu lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wa Serikali za Mitaa wanakua watumishi wa mfano kwa utendaji mzuri.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.