Watendaji watakaoshindwa kukamilisha ujenzi waandike barua za kuacha kazi

Na Mathew Kwembe

Watendaji watakaoshindwa kukamilisha ujenzi waandike barua za kuacha kazi

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI), Mheshimiwa George Simbachawene, amewataka wahandisi, maofisa manunuzi na wahasibu wa Manispaa zote nchini, ambao hawatakamilisha kazi ya ujenzi wa majengo ya Shule za Sekondari, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na ujenzi wa matanki ya maji, hadi kufikia Desemba 30, mwaka huu, kuandika barua ya kuacha kazi wenyewe.

Watendaji ambao watatakiwa kuwajibika kabla ya kuwajibishwa ni wale wa halmashauri zilizo na Shule za Sekondari 528 nchini, ambazo zinanufaika na mradi wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Shule ya Sekondari (MMES) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa asilimia 30.

Waziri Simbachawene alitoa agizo hilo juzi wakati wa ziara ya kukagua miradi iliyopo katika Shule za Jiji la Dar es Salaam na kukuta baadhi ya shule zikiwa ziko hatua ya msingi wakati miradi hiyo ikitakiwa kukamilika Desemba 30, mwaka huu.

Alisema watendaji wengine ambao watahusika kujieleza kukwama kwa miradi hiyo ni maofisa elimu na wakurugenzi wa halmashauri zote zilizonufaika na miradi hiyo.

"Nawahakikishia hii miradi itaondoka na watu, wengine watasherehekea mwaka mpya vibaya, kwa sababu fedha zilishatolewa za kuendesha ujenzi wa majengo haya, lakini hadi leo kuna Shule hazijakamilisha na ukiuliza sababu ni nini, unaambiwa ni mabishano kati ya Ofisa manunuzi na Mhandisi ambao wanauchelewesha, sasa endeleeni kubishana na mchezo mnaocheza lakini haya majengo nayataka Desemba 30 mwaka huu, ukiona huwezi kumaliza andika barua mwenye kabisa ya kuacha kazi kabla sijakufikia," alisema Mheshimiwa Simbachawene.

Pia aliwataka wakuu wa mikoa wote nchini na wakurugenzi wa halmashauri zote kusimamia kikamilifu miradi hiyo ambayo inagharamu Sh. bilioni 158 zilizotolewa na Benki ya Dunia huku Serikali ikichangia asilimia 70, ili ikamilike kwa wakati na kabla ya kuanza mradi mwingine wa awamu ya tatu.

"Watu ambao hamtapona katika hili ni maofisa manunuzi na wahandisi, wakurugenzi nao nitaangalia ameingia lini kazini lakini wahasibu nao watahusika katika hili, nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini, kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili ya mradi huu wa MMES na MARAS na nyie mpo kikaangoni, haya majengo yakamilike mwaka huu," alisema Simbachawene.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Pemba mnazi, wilayani Temeke, alikuta ujenzi wa nyumba za walimu ukiwa kwenye msingi wakati kiasi cha Sh. milioni 289 kilishatolewa kwa ajili ya kazi hiyo.

"Leo sitaki kuchuma dhambi ya kumfukuza mtu kazi ila nataka niwape siku 60 tu, haya majengo yawe yamekamimilika kama tatizo ni mkandarasi mbadilisheni ili kazi hii ikamilike, wahandisi jengeni mahema mkae site (eneo la kazi) mfanye kazi usiku na mchana, mbona wachina wanafanya hivyo wakati wa kujenga nyie mnashindwa nini au mnataka kukaa tu ofisini?" alihoji Waziri Simbachawene.

Aidha, Mheshimiwa Simbachawene aliwashukia wahandisi walioajiriwa na serikali kwa kushindwa kusimamia kazi hiyo kikamilifu baada ya kubaini kuwa majengo yaliyokamilika yana ufa.

Alihoji sababu ya wahandisi kushindwa kusimamia kazi walizosomea licha ya elimu waliyo nayo na ikizingatiwa kuwa gharama za majengo hayo zilitolewa na wao wenyewe.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.