Waziri Simbachawene afafanua agizo lake kwa Wakuu wa Mikoa

Na Mathew Kwembe

Waziri Simbachawene afafanua agizo lake kwa Wakuu wa Mikoa

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amesema agizo alilolitoa hivi karibuni la kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kupita mashuleni lililenga kwa viongozi hao kukagua maendeleo ya wanafunzi darasani na siyo kuwakagua walimu jinsi wanavyofundisha.

Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Mungui, na Kidenge katika kata ya Pwaga, na vijiji vya Ilamba na Mtamba katika kata ya Rudi wilayani Mpwapwa Waziri Simbachawene alisisitiza kuwa ni lazima kwa wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na Viongozi wa Halmashauri kujenga utamaduni wa kupita madarasani kuona kama wanafunzi wanapata elimu kama ilivyokusudiwa na serikali.

"Sikusema wawakague walimu, bali waangalie je wanafunzi wanafundishwa? Na kama wanafundishwa wanafundishwa vizuri? Na kinyume cha kuangalia ni kuona kama wanafunzi wanajua kusoma na kuandika vizuri," alisema.

Waziri Simbachawene aliongeza kuwa kusoma na kuandika hakuhitaji mtu aliyesomea taaluma hiyo kuweza kumjua motto kama anajua kusoma na kuandika.

"Hili ni jukumu letu sisi sote. Hivi karibuni nilikwenda katika shule moja na kukuta watoto wa darasa la sita, walimu wapo wanane, lakini watoto wale hawajui kusoma na kuandika," alisema.

Alisema kuanzia mwezi wa nane mwaka huu serikali imekuwa ikitoa posho kwa walimu wakuu wa shule za msingi, wakuu wa shule za sekondari na wakaguzi wa elimu kata wamekuwa wakipewa shilingi laki mbili kila mwezi kwa ajili ya kuwapa motisha walimu na wakaguzi lakini licha ya motisha hiyo amebaini kuwa zipo baadhi ya shule nchini watoto hawajui kusoma na kuandika vizuri.

Aidha Waziri Simbachawene aliwataka watendaji katika halmashauri kuhakikisha kuwa wanapanga mipango yao katika bajeti za halmashauri kulingana uhalisia wa mahitaji ya halmashauri husika ili waweze kuyafikia malengo yao waliyojiwekea.

Waziri Simbachawene aliyasema hayo baada ya kutembelea shule ya Msingi ya Maswala iliyopo katika Kijiji cha Maswala kata ya Pwaga wilayani Mpwapwa kuwa na madarasa matatu na nyumba moja tu ya mwalimu na upungufu mkubwa wa madawati, hali iliyopelekea uongozi wa halmashauri hiyo kuwahamisha wanafunzi wa kuanzia darasa la nne hadi la saba katika shule ya msingi ya Pwaga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mheshimiwa Donath Sesine Ng’hwenzi alisema kuanzia sasa halmashauri hiyo haitakuwa tayari kupitisha fedha katika mradi ambao ama umetekelezwa vibaya au haujakamilika.

Mheshimiwa Ng’hwenzi alitolea mfano wa mkandarasi aliyelipwa shilingi milioni 48 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati wa Singonali na kisha akaondoka bila ya kukamilika kwa mradi huo.

Alisema kuwa halmashauri hiyo haitakuwa tayari kulipa fedha au kuona mradi mbovu ukitekelezwa katika halmashauri hiyo bila wao kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.